Zarif amhutubu Trump: Usiingilie masuala ya nchi zingine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60480-zarif_amhutubu_trump_usiingilie_masuala_ya_nchi_zingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaka rais wa Marekani Donald Trump akome kuingilia masuala ya nchi zingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2020 22:11 UTC
  • Zarif amhutubu Trump: Usiingilie masuala ya nchi zingine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaka rais wa Marekani Donald Trump akome kuingilia masuala ya nchi zingine.

Katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya katika Ikulu ya Marekani, White House na pasi na kuashiria ugaidi wa kiuchumi anaofanya dhidi ya wananchi wa Iran wakati huu wa janga la corona, Trump amedai kwamba Marekani iko tayari kuleta misaada nchini Iran.

Na licha ya Marekani yenyewe kukabiliwa na matatizo chungu nzima pamoja na uhaba wa vifaa vya tiba na afya kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona, Trump amedai pia kuwa, ikiwa Iran itatoa ombi, atatuma Tehran maelfu ya vifaa vya kupumulia.

Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, rais wa Marekani vilevile amedai kwamba, Iran sasa ni nchi iliyobadilika na akaongezea kwa kusema: "Wanataka (Wairani) wafikie makubaliano. Ninavyohisi, yeye (John Kerry) anawaambia subirini, huenda Trump akashindwa (katika uchaguzi) na nyinyi mkaweza kufanya mazungumzo.

Kufuatia matamshi hayo ya uropokaji aliyotoa Trump, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, Tehran haifanyi mashauriano na mwanasiasa yeyote wa Marekani, na akamhutubu Trump: Kitu pekee unachopaswa kufanya ni kwamba, uache kuingilia masuala ya nchi zingine, hasa Iran.

Katika jibu lake hilo alilotoa kupitia ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Dakta Zarif vile vile amesema kuhusu madai ya Trump kuwa eti tayari kutuma mashine za kupumulia hapa nchini, kwamba kuanzia mwezi ujao, Jamhuri ya Kiislamu itaanza kusafirisha na kuuza nje ya nchi mashine hizo.

Madai ya rais wa Marekani ya kutaka kuipatia msaada Iran yanatolewa wakati mbali na ugaidi wake wa kiuchumi na wa kitiba dhidi ya wananchi wa Iran, Marekani yenyewe ndiyo nchi yenye hali mbaya zaidi duniani kimaafa hivi sasa katika janga la corona baada ya watu wasiopungua elfu 36 kufariki dunia nchini humo na wengine wapatao laki saba na 39 elfu kuambukizwa kirusi cha COVID-19.../