Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Amini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60594-kiongozi_muadhamu_atuma_salamu_za_rambi_rambi_kufuatia_kuaga_dunia_ayatullah_amini
Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia mwanazuoni mujahid na mwanamapinduzi marhum Ayatullah Ibrahimi Amini ambaye pia alikuwa mwanachama wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2020 06:19 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Amini

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia mwanazuoni mujahid na mwanamapinduzi marhum Ayatullah Ibrahimi Amini ambaye pia alikuwa mwanachama wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Ibrahim Amini, mwanachama wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu aliaga dunia Ijumaa usiku mjini Qum baada ya kuugua kwa miezi kadhaa.

Katika ujumbe wake leo Jumamosi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Amini,  Ayatullah Khamenei ametuma salamu za rambi kwa chuo cha kidini cha Qum, wanafunzi na wapenzi wa mwanazuoni huyo mujahid na kusema: "Umri uliojaa baraka wa mwanazuoni huyu mkubwa ulikuwa katika njia ya elimu, kutafuta na kusambaza maarifa ya Kiislamu na pia jihadi ya kisiasa na kijamii."

Aidha amesema mwanazuoni huyo mwendazake alishika nyadhifa rasmi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kama vile kuwa Imamu wa Swala ya Ijumaa na kuwa  mwanachama wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.

Marhum Ayatullah Ibrahimi Amini

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa hulka ya Ayatullah Amini ni mfano wa ucha Mungu na kutovutiwa na masuala ya kimaada na kidunia.

Kwa upande wake, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye pia ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Amini na kusema: "Faqihi huyu mwanamapinduzi katika umri wake uliojaa baraka, mbali na kuandika vitabu vyenye thamani, pia aliweza kushika nyadhifa muhimu za kisiasa na kijamii, na ameacha kazi zenye thamani na zilizojaa fahari na hivyo kwa yakini ataendelea kubakia katika kumbukumbu za taifa la Iran.