Serikali ya Kenya: Haturuhusu ICC kuchunguza visa vya mashambulizi ya “wahuni”
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140928-serikali_ya_kenya_haturuhusu_icc_kuchunguza_visa_vya_mashambulizi_ya_wahuni
Serikali ya Kenya imekataa wito wa upinzani na mashirika ya kiraia kwa Mahakama ya Kimataifa unaotaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ichunguze ongezeko la ghasia za kisiasa nchini humo katia kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027.
(last modified 2026-08-24T13:43:18+00:00 )
Aug 24, 2026 13:39 UTC
  • Musalia Mudavadi
    Musalia Mudavadi

Serikali ya Kenya imekataa wito wa upinzani na mashirika ya kiraia kwa Mahakama ya Kimataifa unaotaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ichunguze ongezeko la ghasia za kisiasa nchini humo katia kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa idara za usalama na taasisi za sheria nchini humo zina uwezo wa kukabiliana na vitisho hivyo.

Mjadala huo umeibua kumbukumbu za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, ambapo mahakama ya ICC ilianzisha uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata.

Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Nje na Wakenya wanaoishi ng’ambo, Musalia Mudavadi, amesema Kenya imejitolea kuzingatia utawala wa sheria na haina haja ya kupeleka uchunguzi wa uhalifu wa ndani kwenye taasisi za kimataifa.

Alisema Kenya haijawahi kukataa kuheshimu utawala wa sheria, iwe katika uwanja wa kimataifa au ndani ya nchi.

Musalia Mudavadi Aamesema: “Serikali hii imefikishwa katika mahakama za humu nchini mara nyingi. Hatujawahi kukaidi maamuzi ya mahakama; daima tumeyaheshimu.”

Bw Mudavadi amepinga wito wa taasisi za kimataifa kuingilia kati, akisema mahakama za Kenya na idara za usalama zina uwezo wa kukabiliana na ghasia na uvunjaji wa sheria kuelekea uchaguzi wa 2027.

Waziri wa Masuala ya Nje wa Kenya ameikumbusha jinsi Rais William Ruto wa nchi hiyo alivyowahi kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu tuhuma za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kesi dhidi ya Rais Ruto iliondolewa baadaye kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Msimamo huo wa serikali ya Nairobi unatofautiana na ule wa viongozi wa upinzani na mashirika ya kiraia yanayotaka kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu kile wanachosema ni dalili za kuandaliwa ghasia za kisiasa.

Jumatano iliyopita, Muungano wa Upinzani, muungano usio rasmi wa wakosoaji wa Rais Ruto, uliitaka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC kuanza kuchunguza matukio ya hivi majuzi ya ghasia za kisiasa nchini.