Waliopona COVID-19 nchini Iran wafika 87,000; 45 wafariki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60920-waliopona_covid_19_nchini_iran_wafika_87_000_45_wafariki
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, miongoni mwa watu 109,000 walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 hadi leo, zaidi ya 87 elfu wa wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2020 10:56 UTC
  • Waliopona COVID-19 nchini Iran wafika 87,000; 45 wafariki

Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, miongoni mwa watu 109,000 walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 hadi leo, zaidi ya 87 elfu wa wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran amesema hayo leo Jumatatu katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongeza kuwa katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, kumegunduliwa watu wapya 683 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 na kwa msingi huo jumla ya waliomabukizwa ugonjwa huo wa corona Iran  hadi sasa ni 109,286.

Kadhalika  ameashiria kufariki dunia wagonjwa 45 wa COVID-19 nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,685 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huo hatari.

Mgonjwa wa COVID-19 akipata matibabu Iran

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran amesema hadi sasa kumefanyika vipimo 600,000 vya COVID-19 katika maabara za Iran na kuongeza kuwa, asilimia 30 ya wagonjwa wapya wamelazwa na asilimia 70 waliosalia wametibiwa na kuondoka hospitalini pasina kulazwa.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, jumla ya watu milioni 4.2 wameambukizwa COVID-19 kote duniani na wengine 284,000 wamepoteza maisha huku milioni 1.5 wakipata afueni.