Zarif: Iran imepiga hatua kubwa katika miradi yake ya nyuklia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa katika miradi yake ya nyuklia.
Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari wakati akijibu swali kuhusu je, kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kumeathiri shughuli za nyuklia za Iran au la na huku akiashiria kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kama kamawaida na shughuli zake za amani za nyuklia amesisitiza kwamba, madai yanayotolewa na Marekani ni ya kipuuzi mno na wala si jambo jipya.
Ameongeza kuwa, watu wanaowashawishi watu wengine wanywe na kujidunga vitakasaji vya corona ili kujisafisha na kutopata ugonjwa huo (akimkusudia rais wa Marekani Donald Trump) si jambo la ajabu kwao kudai hivi sasa kuwa bado ni wanachama wa makubaliano ambayo wamejitoa na kuandika barua rasmi kwamba si wanachama tena wa mapatano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, waitifaki wote wa Marekani wametangaza kuwa, hoja zinazotolewa na nchi hiyo kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA hazikubaliki na amejibu majigambo ya Brian Hook mjumbe maalumu wizara ya mambo ya nje ya Marekani katika masuala ya Iran aliyedai kuwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA yatakuwa yamevunjika kabisa kabla ya uchaguzi wa rais nchini Marekani kwa kusema, kadhia ya JCPOA haimuhusu ndewe wala sikio Brian Hook, kilicho muhimu kwa mapatano hayo ni wajumbe wake yaani Iran na pande zilizobakia kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.