Iran yakosoa barua ya vitisho ya Trump kwa Shirika la Afya Duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61106-iran_yakosoa_barua_ya_vitisho_ya_trump_kwa_shirika_la_afya_duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema barua ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia haina umuhimu wowote na imeandikwa katika wakati usiofaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2020 22:06 UTC
  • Iran yakosoa barua ya vitisho ya Trump kwa Shirika la Afya Duniani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema barua ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia haina umuhimu wowote na imeandikwa katika wakati usiofaa.

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma jana Jumatano kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, "ingawaje afya ya dunia ipo hatarini hivi sasa, na mataifa ya dunia yanahitaji ushirikiano na uongozi uliojikita katika sayansi wakati huu kuliko wakati wowote mwingine ule, lakini barua ya Rais wa Marekani imeingilia utendajikazi na uhuru wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO."

Katika barua hiyo ya vitisho kwa Tedros Adhanom Gabrayesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia na ambayo imekosolewa vikali katika kona mbalimbali za dunia, Trump alisema Marekani itaikatia misaada WHO kikamilifu iwapo haitapiga hatua kubwa za kujiboresha ndani ya siku 30 zijazo.

Kabla ya hapo, Dakta Kamal Kharrazi Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza udharura wa kukabiliana na uingiliaji wa kisiasa wa madola makubwa duniani katika asasi za kimataifa kama Shirika la Afya Duniani (WHO).

Zaidi ya Wamarekani milioni moja na laki tano wameambukizwa virusi vya corona, huku wengine zaidi ya 90,000 wakiaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 

Alisema ili kudhibiti na kukabiliana na virusi vya corona, kuna haja ya kuwepo mshikamano na ushirikiano wa kimataifa chini ya mhimili wa WHO.

Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetoa radiamali yake kwa barua hiyo ya Trump kwa mkuu wa Shirika la Afya Duniani na kusema kuwa,  Rais huyo wa Marekani kwa kuzilaumu WHO na China kwa janga la corona, anakusudia kuficha uzembe wa serikali yake ulioifanya Marekani iwe muathirika mkubwa zaidi wa mlipuko wa corona duniani.