Iran: Sauti ya waandamanaji nchini Marekani lazima isikilizwe
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kulaani mauaji ya raia wa Marekani wenye asili ya Afrika, imesisitiza kuwa sauti za watu wanaoandamana kulaani ukatili wa polisi ya nchi hiyo dhidi ya watu weusi lazima isikilizwe.
Katika ujumbe uliotumwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesema: Iran imesikitishwa na mauaji ya kutisha ya Wamarekani weusi, sambamba na kulaani ubaguzi wa rangi nchini Marekani, na inazitaka mamlaka husika nchini humo kutenda haki kwa kila kesi."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Marekani inapaswa kuacha tabia yake ya kubinya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.
Hii ni katika hali ambayo, hapo jana polisi nchini Marekani ilimkamata na kumfunga pingu mwanahabari wa Televisheni ya CNN mwenye asili ya Afrika akiwa anarusha ripoti hewani mubashara kuhusu ghasia za kupinga ubaguzi wa rangi huko mjini Minneapolis.
Mtu mmoja ameuawa katika maandamano hayoo ya kulaani ukatili wa polisi katika mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota , na hivi sasa maandamano hayo yameenea katika miji na majimbo mengine ya Marekani.
Maandamano hayo yaliripuka kufuatia mauaji ya kutisha ya raia mweusi. Katika mauaji hayo ya kibaguzi ya polisi wa Marekani Jumatatu iliyopita, afisa mmoja wa polisi mzungu alimuua kwa namna ya kikatili George Floyd (46) Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa kumbana shingo kwa goti la mguu wake wa kushoto. Floyd alikuwa akipiga kelele kwa kusema: "Umenibana shingo siwezi kupumua," "naomba maji" na "usiniue" hadi alipofariki dunia.