Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amuomboleza Ramadhan Shalah
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61464-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_amuomboleza_ramadhan_shalah
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia katibu mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 07, 2020 07:38 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amuomboleza Ramadhan Shalah

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia katibu mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina.

Katika salamu zake za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ramadhan Abdullah Shalah Katibu mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje Iran amesema: "Alikuwa katibu mkuu wa muda mrefu katika uga wa Jihadi na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni, alikuwa shakhsia mwanamapambano Palestina na alipitisha umri wake katika mazingira magumu, kwa ushujaa na kujitolea muhanga. Pamoja na kuwepo hatari na vitisho vyote alitumia umri wake katika njia ya Jihadi, kujitolea katika uga wa muqawama na kuikomboa Palestina na Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu."

Zarif ameongeza kuwa, Ramadhan Abdullah alikuwa mtu mwenye khushuu, msomi, mwanafikra aliyekuwa na fikra za kikurubisha madhehebu za Kiislamu na aliyefahamu kwa kina matukio ya kieneo na dunia.

Marhoum Ramadhan Abdullah

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Ramadhan Shalah alikuwa akisisitiza sana kuhusu umoja wa wananchi na makundi ya Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa ana hamu ya kuona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikistawi kwa sababu ni nguzo ya uungaji mkono kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina. 

Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ameaga dunia hospitalini baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

Taarifa iliyotolea na harakati hiyo imesema kuwa, Ramadhan Shalah ameaga dunia akiwa hospitalini katika mji wa Gaza.