Iran kuwa na jumla ya satalaiti 18 kufikia mwishoni mwa mwaka
Kutokana na kuendelea kuboreka sekta ya anga za mbali ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu inapania kuzalisha satalaiti zaidi na kufikisha jumla ya satalaiti 18 kufikia mwishoni mwaka huu wa Kiirani wa Hijria Shamsia, sawa na Machi 20, mwaka 2021.
Hayo yalisemwa jana Jumapili na Mohammad-Javad Azari Jahromi, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Iran katika kikao cha wazi cha Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), wakati akiwaeleza wabunge kuhusu mikakati na miradi mipya ya wizara hiyo.
Amesema wizara hiyo hivi sasa imejikita zaidi katika masuala mawili: Mtandao wa kitaifa wa habari na mradi wa kiraia wa anga za mbali.
Waziri wa TEHAMA wa Iran amesema, Iran ilikuwa imezalisha satalaiti 3 tu kufikia Machi mwaka 2014, lakini satalaiti zingine saba zikazalishwa na wataalamu wa humu nchini kufikia Machi 2018.
Mohammad-Javad Azari Jahromi amesema taifa hili linapania kuwa na jumla ya satalaiti 18 kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 1399 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imevunja ukiritimba na imefanikiwa kupata uwezo wa kuzalisha na hata kurusha satalaiti zake katika anga za mbali pamoja na kuwepo vikwazo vya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.