Rouhani: Iran itasimama kidete zaidi dhidi ya ubeberu wa Marekani
(last modified Thu, 25 Jun 2020 08:01:32 GMT )
Jun 25, 2020 08:01 UTC
  • Rouhani: Iran itasimama kidete zaidi dhidi ya ubeberu wa Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili litasimama kidete zaidi kukabiliana na sera za kibeberu za Marekani hata kuliko huko nyuma.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo jana Jumatano hapa jijini Tehran, wakati akipokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Korea Kaskazini hapa nchini, Han Song Ou.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, "Marekani ni adui wa Iran na Korea Kaskazini na daima imekuwa ikiyafanyia ukatili mataifa haya mawili. Ni kwa sababu hiyo ndio maana tunapaswa kusimama kidete dhidi ya ubeberu wao kwa nguvu zaidi kuliko huko nyuma."

Rais wa Iran aidha amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (Kaskazini), DPRK kwa maslahi ya watu wa nchi mbili hizo na mataifa ya eneo.

Huku akiashiria kuhusu uhusiano wa kidugu baina ya Korea Kaskazini na Iran tokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Dakta Rouhani amesema anatumai kuwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili baina ya Tehran na Pyongyang utaimarika zaidi.

Kwa upande wake, balozi mpya wa Korea Kaskazini hapa jijini Tehran, Han Song Ou amesema kupambana na ubeberu wa Marekani ni nukta ya pamoja katika uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags