Azimio la kurefushwa vikwazo vya silaha halitaathiri nguvu za kujihami za Iran
Meja Jenerali Hossein Salami Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema vikwazo vya silaha vya maadui havina taathira yoyote katika uuwezo wa kujihami wa Iran.
Meja Jenerali Salami aliyasema hayo mjini Tehran Jumamosi wakati alipotembelea maonyesho ya mafanikio ya Shirika la Utafiti na Jihadi ya Kujitosheleza ya Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC na kuongeza kuwa: "Mifumo yote ya silaha katika Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC imefika katika kiwango cha kujitosheleza na kujitegemea."
Katikaa maonyesho hayo kuliwasilishwa mafanikio ya Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nyuga za vita vya kielektroniki, teknolojia ya habari na mawasiliano, ndege zisizo na rubani na magari ya deraya.
Kadiri muda wa utekelezaji wa kipengee cha kuiondolea Iran vikwazo vya silaha kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unavyokaribia, ndivyo utawala wa Marekani unavyozidisha mashinikizo yake ya kuzuia kutekelezwa azimio hilo lililopasisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Marekani imewasilisha azimio katika Baraza la Usalama ambalo linataka kurefushwa kwa muda usiojulikana vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.
Ili kupasishwa azimio hilo kunahitajika kura 9 za ndio za wanachama 15 wa Baraza la Usalama na pia wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo wasitumie kura ya turufu kupinga azimio hilo. Miongoni mwa wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo ni Marekani tu, ambayo imewasilisha azimio hilo, ndiyo inayoliunga mkono huku Russia, China, Uingereza na Ufaransa zikitangaza kulipinga.
Daryl Kimball Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Kudhibiti Zana za Kivita mjini Washington katika mahojiano na Shirika Rasmi la Habari la Iran, IRNA, amesema: "Kwa kuzingatia matamshi ya wanachama wa Baraza la Usalama itakuwa vigumu sana kwa azimio ambalo limependekezwa na Marekani kupitishwa."
Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimepata fahari kubwa kwa sababu leo vinajizalishia ndani ya nchi zana za kujihami na si tegemezi hata kidogo kwa nchi za kigeni.
Moja ya sekta muhimu ambazo Iran imeweza kujitosheleza ni katika uundaji makombora na hii ni sababu muhimu ya kuweza kuzuia na kukabiliana na vitisho vya maadui.
Diyako Husseini, Mkurugenzi wa Mpango wa Utafiti wa Kimataifa katika Kituo cha Utafiti wa Kistratijia anasema: "...Katika kipindi hiki ambacho Iran imewekewa vikwazo vya silaha imeweza kuwa na nafasi muhimu na ya kimsingi katika kusambaratisha kundi la kigaidi la ISIS au Daesh. Aidha Iran imeweza kupata uwezo wa kujihami mkabala wa Marekani na hilo limedhihirika baada ya Iran kushambulia kwa makombora kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ainul Assad nchini Iraq. Hatua hiyo ya Iran imeiwezesha kulinda mlingano wa kijeshi katika eneo. Kile ambacho kinaweza kujiri katika jibu kali la Iran iwapo vikwazo vya silaha dhidi yake vitarefushwa ni kutokuwa tena na imani katika maamuzi ya pande kadhaa wala kuheshimiwa mapatano ya kimataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutegemea uwezo wa wasomi na wataalamu wa ndani ya nchi, mbali na kupata ustawi mkubwa katika sekta ya makombora imeweza pia kupata mafanikio makubwa katika kuunda ndege za kivita. Kuhusiana na nukta hii, sambamba na kushadidi mashinikizo ya Marekani ya kutaka vikwazo vya silaha dhidi ya Iran viongezwe, Wizara ya Ulinzi ya Iran hivi karibuni ilikabidhi Jeshi la Anga la Iran ndege tatu za kivita aina ya Kauthar (Kowsar).
Serikali ya Marekani ambayo inatekeleza mashinikizo ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Iran bado haijaweza kufikia malengo yake dhidi ya nchi hii na kwa hivyo bila shaka haitaweza kufikia malengo yake katika kuiwekea Iran vikwazo vya silaha.
Katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuwekewa vikwazo vya silaha, Majeshi ya Iran yamezidi kusonga mbele na kustawi katika uga wa zana za kijeshi na silaha. Ni wazi kuwa vikwazo havijaweza kuizuia Iran kusonga mbele katika mkondo wa ustawi na kujitosheleza kijeshi.
Ni kwa kuzingatia uwezo huu wa kitaalamu ndio Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema: Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC kina nia ya kuzindua mifumo ya kisasa kabisa na ya kustaajabisha ya kiulinzi. Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC kimejizatiti vilivyo kwa silaha zake zenyewe na za kisasa ili lisibaki nyuma katika teknolojia zinazozidi kupiga hatua siku baada ya siku duniani.