Iran iko mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi
Msemaji wa Serikali ya Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na kuzuia kuenea ugaidi katika eneo la Asia Magharibi na dunia nzima kwa ujumla."
Ali Rabie Msemaji wa Serikali ya Iran ameyasema hayo Jumanne katika mkutano na waandishi habari ambapo ameashiria namna serikali ya Marekani inavyotafsiri maana ya ugaidi na kuongeza kuwa: "Marekani haina ustahiki wa kisheria wala kimaadili kuainisha maana ya ugaidi."
Rabie amesema Marekani haijapewa idhini na chombo chochote cha kimataifa kuainisha maana ya ugaidi na kuongeza kuwa: "Leo dunia inashuhudia namna ambavyo, si tu kuwa serikali ya Marekani inaunga mkono makundi ya kigaidi na wanaowapa himaya magaidi, bali pia yenyewe ni serikali ya kigaidi."
Msemaji wa Serikali ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni adui mkubwa zaidi wa makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada Asia Magharibi na kuongeza kuwa iwapo Marekani haingekuwa inaunga mkono magaidi, idadi kubwa ya watu katika eneo hawangefurushwa makwao au kuuawa.
Rabie halikadhalika amesema kueneza ugaidi ni kati ya sera za undumakuwili za Marekani na kuongeza kuwa: "Hakuna shaka kuwa, Jamhuri ya Kiislmau ya Iran imezuia kuenea ugaidi katika eneo na dunia."