Qalibaf: Iran itasimama kidete mbele ya kujitakia makuu IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62014-qalibaf_iran_itasimama_kidete_mbele_ya_kujitakia_makuu_iaea
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema: "Jamhuri ya Kiislamu itasimama kidete kukabiliana na kujitakia makuu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) .
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2020 03:23 UTC
  • Qalibaf: Iran itasimama kidete mbele ya kujitakia makuu IAEA

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema: "Jamhuri ya Kiislamu itasimama kidete kukabiliana na kujitakia makuu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) .

Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo leo Jumapili katika kikao cha bunge ambapo ameashiria azimio la hivi karibuni dhidi ya Iran ambalo lilitolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kuongeza kuwa: "Iran haitawaruhusu kufanya lolote watakalo katika kukamilisha msururu wa taarifa za kijasusi za nchi hasimu."

Mnamo 19 Juni, Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ilipasisha azimio la kisiasa dhidi ya Iran ambalo lilipendekezwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Azimio hilo lilipasishwa pamoja na kuwa lilipingwa na baadhi ya nchi zikiwemo Russia na China.

Qalibaf aidha ameashiria sera za Iran za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusema sambamba na kupunguza utekelezaji wa mjukumu yake lakini Iran imeendeleza ushirikiano na IAEA.

Ikumbukwe kuwa mnamo Mei 8 2019, Iran ilianza kupunguza utekelezaji wa ahadi na majukumu yake katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kuvunja ahadi zake na nchi za Ulaya nazo pia kushindwa kutekeleza ahadi zao katika mapatano hayo.

Mnamo Januari 5 Iran ilichukua hatua ya tano na ya mwisho katika kupunguza utekelezwaji wa ahadi zake katika JCPOA na sasa Tehran haina tena vizingiti katika shughuli zake za nyuklia zinazojumuisha urutubishaji madini ya urani kwa kiwango inachokitaka na pia kufanya utafiti na kustawisha miradi yake ya nyuklia.

Kwa mujibu wa vipengee 26 na 36 vya JCPOA, iwapo upande mmoja utashindwa kufungamana na ahadi zake katika mapatano hayo, Iran nayo itakuwa na haki ya kusitisha kikamilifu au kidogo utekelezaji wa ahadi zake.