Zarif: EU inapaswa kufungamana na wajibu wake katika mapatano ya JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi za Umoja wa Ulaya zinapaswa kufungamana na wajibu wake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA.
Mohammad Javad Zarif amesema hayo jana Jumatatu jioni katika mkutano wa Jukwaa la Mediterranean (MED 2020) uliofanyika kwa njia ya intaneti ambapo ameashiria kuhusu vikwazo shadidi dhidi ya taifa hili kwa zaidi ya miaka 40 na kufafanua kuwa, "ni kwa maslahi ya watu wa Ulaya kwa EU kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika JCPOA."
Kadhalika amesema utawala ujao wa Washington unapaswa kubeba dhima na kulipia hasara na madhara iliyosababishiwa nchi hii na kubainisha kuwa, "haijalishi ni nani atashinda uchaguzi ujao wa Marekani, lakini serikali ijayo ya Washington inapaswa kuchukua hatua za kuifidia Iran kutokana na hasara ilizosababishiwa na US."
Dakta Zarif amesema jambo la msingi na la muhimu kwa utawala ujao wa Marekani ni kubadili mienendo na mitazamo yake mkabala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amegusia kunako ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya taifa hili na kueleza bayana kuwa, "wanaodai kuwa hawajaliwekea taifa hili vikwazo vya dawa wanapaswa kufahamu kuwa, Iran imefungiwa kufanya shughuli za kibenki katika ngazi ya kimataifa, na kwa msingi huo haiwezi kununua dawa nje ya nchi.
Amesema Tehran ilisaini mapatano ya nyuklia ya JCPOA kwa jicho lililo wazi kabisa na ndiposa imetumia barabara mchakato wa kusuluhisha migogoro ndani ya makubaliano.
Waziri Zarif amesema diplomasia ndiyo njia pekee ya kusulihisha migogoro ya kimataifa na kwamba iwapo EU itarejea katika mkondo wa kufungamana na wajibu wake kwenye JCPOA, Iran nayo haitasita kufuata nyayo.