Waandishi habari wa kigeni wataka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe
Waandishi habari wa vyombo vya habari vya kigeni nchini Iran wamalalamikia vikali kuendelea vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika Rasmi la Habari la Iran (IRNA), waandishi habari wa kigeni walioko nchini Iran wamewaandikia barua viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lugha tatu za Kiarabu, Kiingereza na Kifarsi na kubainisha wazi kuwa: "Janga la COVID-19 limezitwika jukumu kubwa na la kihistoria serikali na mataifa la kuhakikisha matibabu bora zaidi yanapatikana kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanadamu. Waandishi hao wa habari wameashiria vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya watu wa Iran na kusema, historia ya Marekani haijawahi kushuhudia vikwazo kama walivyowekewa watu wa Iran. Taarifa hiyo imesema vikwazo hivyo vimewanyima watu wa Iran haki ya kimsingi kabisa yaani haki ya kulinda maisha ambayo imetajwa katika Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu la Disemba 10 1948.
Waandishi hao wa habari wa kigeni walioko Iran wametoa wito kwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza jukumu lao la kihistoria kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya Marekani ili iachilie fedha za Iran zinazozishikilia ili serikali ya Iran iweze kununua dawa, vifaa vya tiba na chakula.

Rais Donald Trump wa Marekani mnamo Mei 8 2018 alichukua uamuzi wa upande mmoja na kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.
Oktoba 2019, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) ilitoa hukumu ya kuitaka Markeani iondoe vikwazo vya vyakula, dawa na misaada ya kibinadamu dhidi ya Iran. Marekani inaendelea kukaidi amri ya mahakama hiyo.