Brigedia Jenerali Nasirzadeh: Vikosi vya Iran havitaruhusu adui kuvamia ardhi yake
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uadui wa miaka 40 wa madola ya kibeberu dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, majeshi ya Iran yamejiandaa kikamilifu na katu hayataruhusu adui kuvamia ardhi ya taifa hili.
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh ameabainisha hali ya kiusalama ya eneo la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kwamba, vikosi vya Iran vikiwa walinzi wa usalama wa nchi vipo katika eneo hili vikiwa imara kabisa na tayari kwa ajili ya kukabiliana na chokochoko yoyote ile ya adui.
Kamanda huyo wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo katika eneo la Ghuba ya Uajemi ikiwa nchi yenye kulinda amani na kwamba, vikosi vya taifa hili vimejizatiti kikamilifu na vikiwa na utayari mkubwa wa kimapigano katu havitaruhusu audi avamie ardhi ya taifa hili.
Kadhalika Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kusimama kidete taifa la Iran mbele ya vitisho na vikwazo vya kidhalimu ndio sababu kuu ya uadui wa madola ya kibeberu dhidi ya taifa hili la Kiislamu.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika miaka ya hivi karibuni Jeshi la Anga la Iran limepata mafanikio makubwa ambayo ni jibu kwa silaha za kisasa zaidi za maadui na washirika wake katika uga wa vita vya kielektroniki.