Mousavi: Vikwazo vya silaha dhidi yake vikirefushwa, Iran itatoa jibu kali
(last modified Sat, 11 Jul 2020 00:43:59 GMT )
Jul 11, 2020 00:43 UTC
  • Mousavi: Vikwazo vya silaha dhidi yake vikirefushwa, Iran itatoa jibu kali

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema iwapo vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vitarefushwa kufuatia mashinikizo ya Marekani basi Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na muafaka.

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi habari mjini Isfahan, kati mwa Iran ambapo ameashiria azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusema Iran imejitolea kushirikiana na wakala huo lakini ifahamike kuwa ushirikiano huo si wa kudumu.

Kuhusiana na mlipuko katika  kiwanda cha urutubishaji madini ya urani  cha mjini Natanz, kati mwa Iran, Mousavi amesema idara za usalama nchini Iran zinachunguza tukio hilo na iwapo itabainika kuwepo wahusika wa kigeni katika kadhia hiyo basi hilo litatangazwa na matokeo yake yataonekana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameashiria kufuatiliwa kisheria mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: "Kamati maalumu ya kufuatilia kadhia hii imeundwa katika Wizara ya Mambo ya Nje na pia idara zingine kama vile Idara ya Mahakama zinafuatilia pia kadhia hiyo."

Jengo ambalo palijiri mlipuko katika kituo cha urutubishaji madini ya urani Natanz

Kuhusiana na hatua ya Marekani kujiondoa katika Shirika la Afya Duniani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema tokea aingie madarakani, Donald Trump amejiondoa katika mikataba kadhaa ya kimataifa. Ameongeza kuwa, wakati dunia inakabiliana na janga la COVID-19, hatua ya Marekani kujiondoa katika WHO inaweza kutathiminiwa kuwa ni ugaidi wa kiafya na kitiba.

 

Tags