Kuwa tayari jeshi la Iran kwa ajili ya kukabiliana na wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62134-kuwa_tayari_jeshi_la_iran_kwa_ajili_ya_kukabiliana_na_wavamizi
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia miaka 40 ya uhasama wa nchi za kibeberu dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusisitzia kuwa, Jeshi la Iran limejitayarisha kikamilifu na halitamruhusu adui kufanya uchokozi wa aina yoyoye dhidi ya ardhi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2020 03:45 UTC
  • Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh
    Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia miaka 40 ya uhasama wa nchi za kibeberu dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusisitzia kuwa, Jeshi la Iran limejitayarisha kikamilifu na halitamruhusu adui kufanya uchokozi wa aina yoyoye dhidi ya ardhi yake.

Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran ametoa ufafanuzi kuhusu hali ya usalama katika Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, jeshi la Jamhuri ya Kiislamu lipo katika eneo hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa kikanda kwa nguvu zake zote.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, usalama wa eneo nyeti la Ghuba ya Uajemi unaweza tu kulindwa kwa ushirikiano wa nchi zote jirani za eneo hilo. Katika mkondo huo huo, Rais Hassan Rouhani alipendekeza mpango wa "Amani ya Hormuz" kwa ajili ya kuimarisha amani na usalama wa eneo hilo wakati alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York mwaka jana wa 2019. Pendekezo hilo la Rais Rouhani lilionyesha kuwa Tehran inafuata siasa na sera za kushirikisha pande kadhaa katika masuala ya kikanda kwa ajili ya kulinda na kuimarisha amani na usalama wa Ghuba ya Uajemi.

Rais Rouhani akihutubia kikao cha Baraza la Usalama, New York

Hali makhsusi ya jiografia ya kisiasa ya eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz inaonyesha kuwa, njia pekee ya kuaminika kwa ajili ya kuimarisha usalama wa kanda hiyo ni kushirikiana nchi jirani za eneo hilo. Hata hivyo Marekani imekuwa ikivuruga amani katika eneo hilo ikitumia vibaraka na wanasesere wake. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanataja malengo matatu ya harakati za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Kwanza ni kufaidika kisiasa na kiuchumi na machafuko yanayotokea katika eneo hilo. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Tunisia, Lutfi al Obeidi anasema: "Marekani inatumia mbinu ya kueneza hofu na propaganda chafu kuhusu Iran kwa ajili ya kudhamini maslahi yake haramu. Washington inazusha fitina na mifarakano katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa shabaha ya kutayarisha mazingira ya kuwekeana mikataba ya mauzo ya silaha na baadhi ya nchi za eneo hilo, kuziburuta nchi za Kiarabu katika meza ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kupeleka mbele mpango habithi wa Muamala wa Karne"

Benjamin Netanyahu na Donald Trump

Lengo la pili ni kwamba, Marekani inataka kuifanya Iran ikabiliwe na changamoto kubwa ya majeshi ya kimataifa kupitia njia ya kuanzaisha mungano wa kijeshi katika eneo la Lango Bahari la Hormuz.

Suala la tatu la kuzingatiwa katika mjadala wa uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi ni njama za kuanzisha changamoto kadhaa za kiusalama katika maeneo ya kandokando ya Iran na kubana uwezo wa kujilinda wa Jamhuri ya Kiislamu kupitia njia ya kudhoofisha uwezo wa makombora yake.

Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, Marekani inatumia mbinu ya kueneza hofu na propaganda chafu dhidi ya Iran ili ijitangaze kama mtetezi wa amani na usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, wakati lengo halisi la Washington ni kuvuruga amani na usalama wa kanda hiyo kwa maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi.

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh

Matamshi yaliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yana ujumbe wa wazi unaosisitiza kuwa, jeshi la Iran litajibu vikali chokochoko na uchokozi wa aina yoyote katika eneo la Ghuba ya Uajemi, na matokeo mabaya ya suala hilo yataelekezwa kwa majeshi hasimu yakiwemo ya Marekani.