Mousavi: Marekani haitafanikiwa kusukuma mbele gurudumu la siasa zake haramu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ubeberu wa Marekani dhidi ya asasi za kimataifa hauwezi kuisaidia kusukuma mbele gurudumu la siasa zake zisizo za kisheria na kwamba, kinyume na mtazamo wa Rais Donald Trump, zama za utawala wa kisheria hazijamalizika.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo ameashiria kuwadia tarehe 14 Julai hapo kesho ambayo ni kumbukumbu ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kukumbusha kwamba, kabla ya kuingia madarakani Rais Donald Trump, baadhi ya masuala katika makubaliano hayo yalikuwa katika mkondo wa kawaida, lakini alipoingia madarakni kiongozi huyo alianza kuchukua hatua na misimamo ambayo sio ya uwajibikaji ambapo aliiondoa nchi yake katika makubaliano hayo muhimu ya kimataifa na kuanza kutekeleza vikwazo dhidi ya Iran katika awamu mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua zilizochukuliwa na Tehran za kupunguza kwa awamu uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya upande wa pili kutotekeleza ahadi zake na kusema kuwa, hatua hizo za Iran hazikiuki makubaliano hayo.
Abbas Mousavi amesema kuwa, Trump anafuatilia suala la kupata ushindi katika uga wa siasa za kigeni ili ajijengee nafasi nzuri katika uchaguzi ujao hapo Novemba, na ndio maana hivi sasa serikali yake inafanya njama za kukwamisha mwenendo wa utekelezaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; hata hivyo kwa mujibu wa azimio hilo kufikia Oktoba 18 mwaka huu vikwazo vyote vya silaha dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa.