Zarif: Marekani inadhalilisha sheria na diplomasia na kuhatarisha usalama wa dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametuma ujumbe kwa mnasaba wa mwaka wa tano wa kufikiwa mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) na kusema: "Kitendo cha Marekani cha kudhalilisha sheria na udiplomasia ni jambo linalohatarisha usalama wa nchi hiyo na dunia kwa ujumla mbali na kuchafua jina la Washington katika uga wa kimataifa."
Katika ujumbe wake kupitia Twitter siku ya Jumanne ya jana, Muhammad Javad Zarif alisema mapatano ya JCPOA yalikuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya muongo uliopita na kwa mara nyingine serikali ya Marekani inakosolewa kwa hatua zake zisizo za kisheria kuhusu mapatano hayo.
Zarif ameashiria kitendo cha Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika mapatano ya JCPOA na kusema: "Tabia ya Marekani ya kukwepa sheria haipaswi kuwa kigezo cha desturi za kimataifa."
Katika ujumbe wake huo wa Twitter Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika kipindi cha miaka mitano, Iran imefungamana na kuheshimu mapatano ya JCPOA ambayo yamekiukwa mara kadhaa na Marekani. Amesema Iran haijawahi kupata himaya iliyoahidiwa na nchi za Magharibi zilizosalia katika JCPOA baada ya Marekani kujiondoa.
Zarif ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Iran, udiplomasia una umuhimu na kwamba: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitamruhusu mbabe adhoofishe maslahi ya Iran kwa kuitisha jamii ya kimataifa.
Baada ya miaka 13 ya mazungumzo magumu ya kimataifa, hatimaye tarehe 14 Julai mwaka 2015 kulifikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Mapatano hayo yalikuwa baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kundi la 5+1 ambalo lilijumuisha Russia, China, Marekani, Uingereza, Ufaransa pamoja na Ujerumani na halikadhalika Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Marekani ilianza kukiuka mapatano hayo katika siku za awali za kuanza kutekelezwa kwake, na baada ya Donald Trump kuchukua hatamu za uongozi ukiukwaji huo ulishika kasi zaidi.
Hatimaya Mei 8 2018, Trump alichukua uamauzi wa upande mmoja wa kukiuka mapatano ya JCPOA. na kutangaza kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa. Baada ya hapo Trump alirejesha vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran.