Wagonjwa zaidi ya 228,000 wa Covid-19 nchini Iran wamepata afueni
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema, watu zaidi elfu mbili waliokumbwa na ugonjwa wa Covid-19 wamegunduliwa nchini, huku idadi ya waliopata afueni ya ugonjwa huo ikipindukia 228,000.
Sima Sadat Lari ameyaeleza hayo leo wakati akitoa takwimu mpya za watu waliokumbwa na virusi vya corona hap anchini Iran na akabainisha kuwa: Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi, katika muda wa saa 24 zilizopita wagonjwa wapya 2,388 waliokumbwa na ugonjwa wa Covid-19 wamegunduliwa hapa nchini, ambapo 1,775 miongoni mwao wamelazwa hospitali na waliosalia wamepatiwa huduma za tiba na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Bi Lari amefafanua kuwa, idadi ya watu waliougua ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran imefikia 264,562 na kutokana na wagonjwa 199 kuaga dunia katika kipindi cha saa 24 zilizopita, jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo hadi sasa imefikia 13,410.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran hadi kufikia leo mchana, wagonjwa 227,561 wamepata afueni na kuruhusiwa kutoka hospitalini na kurejea majumbani.
Hayo yameripotiwa huku idadi ya watu waliokumbwa na virusi vya corona duniani kote ikifikia milioni 13 na laki tano. Miongoni mwa hao, watu watu wasiopungua 581,000 wameshaaga dunia na wengine zaidi ya 7,875,000 wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.../