Aug 24, 2020 11:59 UTC
  • Zarif: Safari ya Mkuu wa IAEA Iran haina uhusiano na 'Snapback Mechanism'

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema safari ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi‎ hapa nchini haina mfungamano wowote na utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran unaofahamika kama 'Snapback Mechanism'.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo Jumatatu na kuongeza kuwa, safari ya Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA inafanyika kufuatia mazungumzo baina ya Tehran na taasisi hiyo ya kimataifa.

Kadhalika Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, "ushirikiano wa Iran na IAEA umejengeka katika misingi ya uwazi. Safari hiyo haina uhusiano wowote na utaratibu wa Snapback Mechanism."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaja utaratibu wa 'Snapback Mechanism' ambao ni wa kurejesha vikwazo vyote vya UN dhidi ya Iran kama isitilahi bandia na ya kupotosha iliyoundwa na Marekani.

Amesema kamwe Jamhuri ya Kiislamu haitaruhusu Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unamiliki silaha za nyuklia katika eneo na umeshawahi kuzitumia, kuyafanyia dhihaka malengo ya IAEA.

Ushirikiano wa Iran na IAEA

Dakta Zarif amebainisha kuwa, nchi 13 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) hivi karibuni zilikataa kuiunga mkono Marekani katika njama zake za kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, na kwamba nchi hizo pia zinaamini kuwa US haina haki ya kujiingiza katika katika mambo yanayohusiano na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Itakumbukwa kuwa, Mei mwaka 2018, Rais Donald Trump alichukua uamuzi wa kuitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini hivi sasa anadai kwamba Washington ina haki ya kutumia  kipengee cha "Snapback Mechanism", ambao ni utaratibu ni wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  

Tags