Ndege za kivita za Iran zashiriki kwa ufanisi mkubwa katika luteka
Kamanda wa Kikosi cha la Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ndege za jeshi hilo zinashiriki kwa ufanisi mkubwa katika maneva na luteka ya kijeshi ya pamoja na Walinzi wa Anga ya Velayat-99.
Mtandao wa habari wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umetangaza habari hiyo leo na kumnukuu Kamanda Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh akizungumzia mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ya Walinzi wa Anga ya Velayat-99 na kusisitiza kwamba, kushiriki ndege za kivita za jeshi la Iran kwa kutumia ndege aina ya F4 na F14 na bila ya marubani kunaendelea hivi sasa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Aidha amesema kuna ulazima wa kikosi cha anga cha jeshi hilo kushiriki kwenye luteka zote za kijeshi zinazofanyika humu nchini na kuongeza kuwa hii ni mara ya pili kwa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kushiriki kwenye maneva ya kijeshi mwaka huu baada ya yale ya pamoja yaliyofanyika kwa jina la Dhulfiqar-99.
Mazoezi ya kitaalamu ya Jeshi la Anga yaliyopewa jina la Walinzi wa Anga ya Velayat-99 yalianza jana Jumatano yakiongozwa na kusimamiwa na kambi kubwa ya Jeshi la Anga la Iran. Lengo la mazoezi hayo ni kunyanua juu uwezo na utayari wa jeshi la Iran kwa kushirikisha vikosi vya Jeshi la Anga na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SEPAH) katika mazingira yanayokaribiana sana na ya vita halisi. Mazoezi hayo yanafanyika katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya nusu ya ardhi ya Iran.