Zarif: Magaidi wa Septemba 11 walitoka katika nchi anayoipenda Pompeo
(last modified Wed, 13 Jan 2021 07:59:07 GMT )
Jan 13, 2021 07:59 UTC
  • Zarif:  Magaidi wa Septemba 11 walitoka katika nchi anayoipenda Pompeo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa radiamali kuhusu madai yasiyo na msingi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye ameifungamanisha Iran na kundi la kigaidi la Al Qaeda na kusisitiza kuwa: "Magaidi wote wa Septemba 11 walitoka katika nchi anazozipenda Mike Pompeo katika Mashariki ya Kati (Asia Magharibi).

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumanne na kuandika: "Kuanzia kuitangaza Cuba kuwa nchi inayounga mkono ugaidi hadi kutangaza nyaraka zinazodaiwa kuwa zilikuwa za siri kuhusu Iran na madai kuhusu Al Qaeda, huyu bwana wa 'tulidanganya, tulihadaa na tuliiba' anamaliza kazi yake iliyojaa maafa kwa kueneza hadaa za ngoma za kivita."

Zarif amekumbusha kuwa, hakuna atakayehadaika kwani magaidi wote wa Septemba 11 walikuwa ni kutoka nchi anazozipenda Mike Pompeo katika eneo la Mashariki ya Kati na miongoni mwazo, Iran haimo.

Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amewahi kunukuliwa akisema: "Mimi nilikuwa Mkuu wa CIA (Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani), tulidanganya, tulihadaa na tuliiba..."

Mike Pompeo

Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Pompeo alitoa madai yasiyo na msingi kuwa Iran ni kituo cha Al Qaeda na kuongeza kuwa idadi kubwa ya wanachama wa Al Qaeda walihamia Iran baada ya matukio ya Septemba 11.

Katika matukio ya Septemba 11 mwaka 2001, karibu Wamarekani 300 waliuawa na wengine zaidi ya elfu sita walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Bunge la Congress la Marekani, na ambao ulitayarishwa miezi kadhaa baada ya tukio la Septemba 11, watu 15 kati ya 19 walioteka ndege zilizohusika katika hujuma za mashambulio hayo ya Septemba 11 walikuwa ni raia wa Saudia, wawili walikuwa raia wa Umoja wa Falme za Kiarabu  na wote walikuwa wanafungamana na maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili ambao waliwapa msaada wa kilojistiki na kifedha.