Mashirika makubwa duniani yawania kuingia katika sekta ya gesi na mafuta Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i6625-mashirika_makubwa_duniani_yawania_kuingia_katika_sekta_ya_gesi_na_mafuta_iran
Kufuatia kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, hivi sasa mashirika makubwa ya dunia yako mjini Tehran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sekta za mafuta, gesi na petrokemikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2016 02:50 UTC
  • Waziri wa Mafuta Iran, Bijan Namdar Zangeneh
    Waziri wa Mafuta Iran, Bijan Namdar Zangeneh

Kufuatia kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, hivi sasa mashirika makubwa ya dunia yako mjini Tehran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sekta za mafuta, gesi na petrokemikali.

Wakurugenzi wa mashirika zaidi ya 880 kutoka nchi 38 wameshiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Gesi, Mafuta na Petrokemikali. pambizoni mwa maonyesho hayo, wakurugenzi wa mashirika ya kigeni wamefanya mazungumzo ya kina na maafisa wa ngazi za juu wa Iran kuhusu kushiriki katika miradi ya mafuta, gesi na petrokemikali nchini Iran.

Bijan Namdar Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Iran siku ya Jumamosi katika kikao cha pamoja na washikadau wa sekta ya mafuta nchini Iran aliashiria mazingira yaliyojitokeza baada ya kuondolewa vikwazo na kusema mashirika mengi ya kigeni yanataka kuimarisha uhusiano na Iran. Amesema hivi sasa Iran inauza mapipa milioni 2.450 ya mafuta kila siku.

Rukn Din Jawadi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Mafuta la Iran amesisitiza kuwa, katika kustawisha sekta yake ya mafuta, Iran haitegemei mashirika ya kigeni. Amebainisha kuwa Iran itajitahidi kuimarisha sekta yake ya mafuta na gesi kwa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi.

Jawadi amesema Maonyesho ya Kimataifa ya Gesi na Mafuta ni fursa nzuri kwa ajili ya kujuana mashirika ya Iran na kigeni ili kwa njia hiyo Iran iweze kupiga hatua ya kujitosheleza.

Aidha Behzad Mohammadi Mkurugenzi wa Shirika la Uhandisi wa Mafuta amesema Maonyesho ya Kimataifa ya Gesi na Mafuta nchini Iran ni fursa nzuri ya kubadilishana teknolojia na mashirika ya kigeni.

Mohammadi amesisitiza kuwa, Kituo cha Utafiti wa Mafuta cha Iran hadi sasa kimefanya mazungumzo na wawakilishi wa Uingereza, Uholanzi, Ujerumani, Austria, China, Norway, India, Ufaransa, Korea Kusini, Kuwait, Kazakhstan, Uhispani na Italia.

Ali Safari Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli za Mafuta la Iran naye amebaini kuwa, meli za shirika hilo hivi karibuni zitaanza kutia nanga katika bandari za Ulaya. Amesema Meli za Shirika la Mafuta la Iran zinaweza kukidhi mahitaji ya usafirishaji mafuta yote ya Iran katika soko la kimataifa.

Kwingineko Azizullah Ramadhani, mkuu wa masuala ya kimataifa katika Shirika la Kitaifa la Gesi la Iran amesema wakuu wa shirika la Gazprom la Russia wako Tehran kwa ajili ya mazungumzo kuhusu sekta mbali mbali za gesi.

Hali kadhalika ujumbe wa ngazi za juu wa Poland uko Tehran ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati wa nchi hiyo kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uwekezaji katika sekta za mafuta na gesi. Aidha mashirika ya Korea Kusini yametiliana saini mapatano na Iran kuhusu utafiti wa setka ya mafuta.

Maonyesho ya 21 ya Kimataifa ya Gesi, Mafuta na Petrokemikali yalianza Alkhamisi iliyopita mjini Tehran ambapo kuna mashirika 1900 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 38 za dunia. Maoneysho hayo ambayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa yatafungwa rasmi leo mchana.

Inakadiriwa kuwa hifadhi ya mafuta ghafi ya petroli ya Iran katika Ghuba ya Uajemi pekee imefikia mapipa bilioni 100. Iran inatajwa kuwa nchi ya nne kwa utajiri wa hifadhi ya mafuta ghafi ya petroli duniani.

Aidha Iran ina hifadhi ya mita mraba bilioni 187 za gesi asilia katika Ghuba ya Uajemi ambapo hivi sasa ina uwezo wa kuchimba asilimia 75 ya gesi hiyo. Inakadiriwa kuwa Iran ni nchi ya pili duniani kwa hifadhi ya gesi baada ya Russia. Kwa msingi huo Iran ni moja ya nchi muhimu duniani katika sekta ya mafuta na gesi na hivyo inaendelea kuvutia mashirika makubwa ya kimataifa.