Iran yasafirisha kwa wingi matrekta katika nchi za Afrika, Asia
Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kuzalisha Matrekta la Iran amesema nchi hii imeanza kuuza kwa wingi tingatinga katika nchi za Afrika, Asia na Amerika ya Latini.
Abolfath Ebrahimi amesema hayo mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, mbali na kuwa na kampuni za kuzalisha matrekta hapa nchini, lakini Jamhuri ya Kiislamu ina matawi ya kampuni hizo katika nchi nyingine duniani.
Amesema mwaka huu vifaa na suhula zinazozalishwa na kampuni hizo zinatazamiwa kuuzwa kwa wingi si tu kwa nchi za Afrika, Asia na Amerika ya Latini, bali hata kwa nchi zinazopakana na Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema kuongezeka kwa mauzo hayo si tu kutaongeza kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara baina ya Iran na nchi za dunia, bali pia kutabuni nafasi nyingi za ajira baina ya pande zote.
Tingatinga hizo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinatazamiwa kupiga jeki sekta ya kilimo katika nchi hizo zilizozinunua.