Salehi: Mkwamo katika mapatano ya JCPOA umeanza kuondoka
(last modified Sat, 03 Apr 2021 07:28:47 GMT )
Apr 03, 2021 07:28 UTC
  • Salehi: Mkwamo katika mapatano ya JCPOA umeanza kuondoka

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, mkwamo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA umeanza kuondoka na kuongeza kuwa, kwa vile hivi sasa mazungumzo kuhusu JCPOA yameingia katika hatua ya kiufundi na yameshatoka kwenye mivutano ya awali, maana yake ni kwamba mkwamo katika mazungumzo hayo umeanza kuondoka.

Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mahojiano na mtandao wa kijamii wa "Clubhouse" na kuongeza kuwa, mazungumzo ya kiufundi kuhusu JCPOA yanatarajiwa kufanyika wiki ijayo mjini Vienna, Austria, na mazungumzo hayo yatajikita katika masuala ya kisheria na kisiasa ya makubaliano hayo.

Mkuu huyo wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran pia amesema, kikao cha jana Ijumaa cha kamisheni ya JCPOA kimetoa fursa ya kuandaliwa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kiufundi ya kisiasa na kisheria ya mapatano hayo.

 

Kikao cha jana cha kamisheni ya JCPOA kilifanyika chini ya uenyekiti wa Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Hatua za Nje za Umoja wa Ulaya akimwakilisha Josep Borrell, mratibu wa masuala ya mapatano ya JCPOA wa Umoja wa huo na Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Timu ya Iran katika mazungumzo hayo.

Kikao hicho kilizungumzia pia uwezekano wa kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA na kilijadili pia uhakikisho wa pande zote wa kutekeleza kikamilifu vipengee vya mapatano hayo ya kimataifa.

Dk Salehi amesema, Iran haitoacha haki yake yoyote ya nyuklia na kusisitiza kuwa, mjadala wa changamoto yetu na Magharibi si suala la nyuklia, bali mjadala huo ulianza tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Tags