Khatibzadeh: Kikao cha 4+1 cha Vienna kitajadili jinsi ya kutekeleza JCPOA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa, ajenda ya kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya mapatano ya JCPOA ni kujadili jinsi ya kutekeleza vipengee vyote vya mapatano hayo ya nyuklia.
Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, kikao cha kesho cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA hakina tofauti ya vikao vingine vya kabla yake vya kamisheni hiyo na kuongeza kuwa, ajenda kuu ya kikao hicho ni suala la kuondoa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na jinsi pande mbili zitakavyotekeleza majukumu yao ndani ya makubaliano ya JCPOA.
Kauli hiyo imekuja baada ya kutolewa taarifa kadhaa za maafisa wa nchi za Magharibi kuhusu kujumuishwa kwenye mazungumzo hayo mipango ya makombora Iran na sera za kikanda jamhuri ya Kiislamu, wakati sharti la Iran la kurudi kwenye utekelezaji kamili wa JCPOA ni kuondolewa kikamilifu na kwa mpigo vikwazo ilivyowekewa na Marekani na kisha kupata hakikisho la taathira chanya za hatua hiyo; na si uondolewaji wa hatua kwa hatua.
Kuhusu madai yaliyotolewa na gazeti la Wall Street Journal juu ya kumefikiwa mapatano huko Vienna, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema, swali kwamba kundi la 4+1 litazungumza vipi na wapi na Marekani linawahusu wanachama wa 4+1 peke yao.
Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa, suala hilo liko wazi la kwamba vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa na kisha kupatikane hakikisho la taathira chanya za hatua hiyo; wakati huo Iran itakuwa tayari kutekeleza kikamilifu vipengee vyote vya JCPOA.
Hapo kabla, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa alisisitiza kuwa "kuhusu pande zote kurudi kwenye utekelezaji wa JCPOA, tutafanya mazungumzo na kundi la 4+1 tu na hatutakuwa na mazungumzo yoyote ya ana kwa ana au yasiyo ya ana kwa ana na Marekani."
Kikao cha msimu cha kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kitafanyika kesho mjini Vienna kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Iran na nchi zinazounda kundi la 4+1.