Araqchi: Kumefikiwa mapatano ya kuondoa aghalabu ya vikwazo dhidi ya Iran
(last modified Sun, 02 May 2021 07:36:00 GMT )
May 02, 2021 07:36 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kikao cha jana cha Tume ya Pamoja ya Mapatano ya Nyuklia ya JCPOA na kusema kikao hicho kimefikia mwafaka kuhusu kuondolewa Iran vikwazo.

Sayyid Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo Jumamosi baada ya kumalizika duru nyingine ya kikao cha tume hiyo ya pamoja ya JCPOA huko Vienna Austria. Amesema pande husika zimeafikiana kuhusu kuondolewa vikwazo aghalabu ya watu na taasisi katika orodha ya vikwazo ya Marekani. Aidha amesema mazungumzo zaidi yatafanyika kuhakikisha kuwa vikwazo vyote vinaondolewa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wawakilishi wa kundi la 4+1 ambalo linaundwa na nchi za Ufaransa, Russia, China, Uingereza na Ujerumani pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya.

Timu za mazungumzo hayo pamoja na majopokazi yake yamekuwa na vikao nyeti na vigumu hivi karibuni yakijadili matini za masuala muhimu; na kikao cha jana kilikuwa ni mwendelezo wa vikao hivyo ambavyo lengo lake ni kujaribu kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hususan kadhia ya kuondolewa vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa jana ni pamoja na kutathmini na kufikia natija jumla majopokazi matatu ya nyuklia kuhusu vikwazo na namna ya kuzungumzia utaratibu wa kuthibitisha kama makubaliano yaliyofikiwa yametekelezwa. 

Duru zinadokeza kuwa, licha ya kuwa mazungumzo hayo kuwa magumu lakini kumepigwa hatua nzuri na kwamba, pande husika zimo katika hatua ya kuandaa muswada wa mapatano.

Imeafikiwa kuwa washiriki katika mazungumzo ya Vienna warejee katika nchi zao kwa ajili ya mashauriano na wakutana tena Ijumaa kuendeleza mazungumzo.

Tags