Zarif aonesha hisia zake kufuatia miaka mitatu ya kujitoa Marekani katika JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonesha hisia zake kufuatia miaka mitatu ya kujitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba miaka mitatu iliyopita, kulizuka "kinyago cheusi" katika ahadi za Marekani ndani ya ndani ya azimio nambari 2231 na mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Dk Mohammad Javad Zarif aliandika hayo jana Jumamosi katika ukurasa wake wa Twitter na kuongeza kuwa, wakati tunafanya juhudi za kuyafufua makubaliano ya JCPOA huko Vienna, ni jambo la lazima tusisahau, bali tujikumbushe wakati wote chanzo cha matatizo yaliyopo.
Amegusia jinsi Marekani ilivyozusha matatizo hayo kwa kujitoa kijeuri kwenye mapatano ya JCPOA wakati wa urais wa Donald Trump hapo tarehe 8 Mei, 2018 na kuandika: Miaka mitatu iliyopita, "kinyago cheusi" kilijitokeza katika ahadi za Marekani ndani ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameandika, jukumu lote hivi sasa liko kwenye mabega ya serikali ya Marekani.
Amesema, rais wa hivi sasa wa Marekani, Joe Biden anapaswa kuchukua maamuzi ya busara ya kuifanya nchi hiyo isiendelee kuvunja sheria.
Marekani ndiyo iliyojitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kukanyaga ahadi zake ndani ya mapatano hayo, hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ililazimika kutumia haki yake ya kupunguza baadhi ya ahadi zake ndani ya makubaliano hayo kama vinavyosema vipengee vyake.
Iran imesema wazi kwamba, mara Marekani itakaporejea kwenye mapambano hayo, nayo haitokuwa na sababu yoyote ya kutotekeleza ahadi zake zote ndani ya JCPOA.