Rais Rouhani: Usalama na Uthabiti nchini Iraq ni usalama Iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema usalama na uthabiti nchini Iraq ni sawa na usamala nchini Iran na amesisitiza kuhusu ushirikiano wa nchi mbili katika kukabiliana na taharui za makundi ya wakufurishaji na magaidi.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi ambapo awali amempongeza yeye na taifa la Iraq kwa mnasaba wa siku kuu ya Idul Fitr na kuongeza kuwa: "Kundi la kigaidi la Daesh lingali hatari kwa usalama wa eneo na hivyo ni dharura kwa nchi hizi mbili kushirikiana katika kukabiliana na kundi hilo la kigaidi.
Rais Rouhani amesema Marekani ina undumakuwili katika madai yake ya vita dhidi ya ugaidi kwani utendaji wake katika mpaka wa Iraq na Syria una utata.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza msimamo wa Iraq kuhusu Palestina hasa kulaani jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa, inatazamiwa kuwa Iraq itatumia ushawishi wake katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu ili kuhakikisha jumuiya hiyo inachukua misimamo amilifu zaidi kuhusu Palestina.
Rouhani pia amesisitiza kuhusu udharura wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Iraq katika nyuga mbali mbali za kisiasa na kiuchumi na pia ushirikiano katika masuala ya kieneo .
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi pia ameipongeza serikali na watu wa Iran kwa mnasaba wa siku kuu ya Idul Fitri huku akilaani vikali jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina. Aidha amesema mazungumzo yanafanyika na viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu-OIC- na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ili kuhakikisha kuwa taasisi hizo mbli zinachukua msimamo imara kuhusiana na kadhia ya Palestina. Aidha amesisiriza kuhusu kuendeleza vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh katika eneo. Aidha amesema serikali ya Iraq itachukua hatua dhidi ya wale waliohujumu ofisi za kidiplomasia nchini Iraq hivi karibuni.