Araqchi: Mapatano yamefikiwa kuhusu kuondolewa asilimia 95 ya vikwazo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa mapatano yamefikiwa kuhusu kuondolewa asilimia 95 ya vikwazo.
Sayyid Abbas Araqchi ambaye alikuwa kizungumza katika kikao cha Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) baada ya mauzungumzo ya jana ya Vienna ametoa ripoti kuhusu mwenendo wa mazungumzo hayo na kusema, asilimia 95 ya vikwazo vyote imeondolewa.
Shahriyar Heydari mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran ameliambia shirika la habari la Iran Press kwamba: Araqchi ametangaza kuwa, asilimia tano ya vikwazo iliyosalia inaendelea kujadiliwa kwenye mazungumzo na kwamba vikwazo hivyo pia vitaondolewa.
Heydari amesema kuwa, vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran sawa vile vinavyohusu watu binafsi au taasisi mbalimbali vinajadiliwa na kwamba asilimia kubwa ya vikwazo vya taasisi vimeondolewa.
Heydari amesema anatajia kwamba kuondolewa vikwazo hivyo kuwatauwa na matokeo mazuri katika maisha ya wananchi wa kawaida na taasisi za serikali.
Kwa wiki kadhaa sasa wawakilishi wa Iran na kundi la 4+1 ambalo linajumuisha China, Russia, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya wamekuwa wakifanya mazungumzo Vienna kwa lengo la kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yamedorora baada ya Marekani kujiondoa na kuiwekea Iran vikwazo.
Tehran inasisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo viliwekwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump, ni hatua ya dharura kwa ajili ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA.