May 29, 2021 12:32 UTC
  • Brigedia Jenerali Qaani: Wazayuni waondoke mara moja katika ardhi za Wapalestina

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wakati umefika kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka katika ardhi za Wapalestina unaozikalia kwa mabavu haraka iwezekanavyo.

Brigedia Jenerali Ismail Qaani amesema hayo leo Jumamosi hapa mjini Tehran, katika kumbukumbu za kuadhimisha Arubaini ya Brigedia Jenerali Mohammad Hosseinzadeh Hijazi, aliyekuwa Naibu Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH ambaye aliaga dunia mwezi Aprili mwaka huu akiwa na umri wa miaka 65, kutokana na mshtuko wa moyo.

Brigedia Jenerali Qaani ameeleza bayana kuwa, Wazayuni wanapaswa kuondoka na kuzikabidhi ardhi walizozighusubu kwa Wapalestina, na warejee makwao huko Marekani na Ulaya. Amesema, "Nawashauri Waisraeli ambao waliuza majumba yao huko Marekani na Ulaya na kwenda Palestina, warejee walikotoka kabla ya bei za majumba hayo hazijaongezeka maradufu."

Baadhi ya makombora ya harakati ya muqawama ya HAMAS

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel hauwezi tena kulemaza mapambano ya Wapalestina kwa risasi na silaha, na kwamba kambi ya muqawama inazalisha silaha zote inazohitaji ndani ya maeneo yake ya kijiografia, yakiwemo makombora 3000 iliyoyavurumisha kuelekea Israel katika vita vya siku 12 vya hivi karibuni.

Hapo jana pia katika mahojiano na televisheni ya al-Masirah, Brigedia Jenerali Ismail Qaani alisema kuwa, bwabwaja na vitisho vya Wazayuni si kitu kingine bali upumbavu, kwa kuwa hivi karibuni tu Ukanda wa Gaza ambao uko chini ya mzingiro wa miaka mingi wa Israel ulitoa pigo kubwa kwa utawala huo pandikizi.

Ameongeza kuwa, " ni uongo kudai kuwa hakuna anayeweza kuushinda utawala wa Kizayun, hivyo vitisho vya shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni Mossad vya eti linaweza kuanzisha vita dhidi ya Iran, hususan baada ya kushindwa na muqawama wa Wapalestina, ni upuuzi tu."

Tags