Vifaa vya tiba vya Iran vinauzwa katika nchi 44 duniani
Katibu wa Umoja wa Wasafirishaji Nje Vifaa vya Tiba vya Iran amesema kuwa, Tehran inauza vifaa vyake vya tiba kwa nchi 44 duniani.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Bw. Mohammad Reza Kompani akisema hayo leo pambizoni mwa maonyesho ya 19 ya kimataifa ya vifaa vya tiba vya Iran hapa Tehran na kuongeza kuwa: Kila mwaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauza vifaa vya tiba vyenye thamani ya dola milioni 30 kwa nchi 44 duniani na hivi sasa ina mpango wa kutafuta masoko zaidi ya kuuza bidhaa zake hizo.
Amesema, baadhi ya vifaa hivyo vinauzwa barani Ulaya na hususan nchini Ujerumaini na Italia na vyote vina alama ya ubora wa vifaa vya tiba ijulikanayo kwa jina la CE. Amesema, vifaa hivyo vimepata soko katika nchi hizo 44 duniani kutokana na ubora wake na bei yake nafuu.
Ameongeza kuwa, baadhi ya vifaa vya tiba vya Iran vinavyouzwa katika nchi kama vile Ujerumaini, Sweden, Belarus, Malaysia, Czech na Russia hufungwa na kutiwa alama katika nchi hizo hizo.
Maonyesho ya 19 ya kimataifa ya vifaa vya tiba, matibabu ya meno, maabara, uzalishaji madawa na utalii wa masuala ya afya yanaendelea hadi keshokutwa Jumatano hapa mjini Tehran.