Raeisi ataka kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73178-raeisi_ataka_kuimarishwa_uhusiano_wa_iran_na_nchi_za_afrika
Rais wa Iran amesema kiwango cha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Afrika ikiwemo Ghana hakiridhishi na kwamba kuna haja ya kuimarishwa zaidi mahusiano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2021 08:05 UTC
  • Raeisi ataka kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi za Afrika

Rais wa Iran amesema kiwango cha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Afrika ikiwemo Ghana hakiridhishi na kwamba kuna haja ya kuimarishwa zaidi mahusiano hayo.

Sayyid Ibrahim Raeisi amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Utalii wa Ghana, ambaye ni miongoni mwa viongozi kutoka nchi mbalimbali duniani waliowasili hapa Tehran kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais huyo mpya wa Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali ya 13 anayoiongoza itafanya juu chini kuhakikisha kuwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Ghana pamoja na nchi nyingine za Afrika unanyanyuliwa katika kiwango cha juu zaidi.

Kadhalika amemtaka Ibrahim Muhammad, Waziri wa Utalii wa Ghana kuwasilisha ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa rais wa nchi hiyo ya Kiafrika kwamba Tehran ina hamu ya kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili na Accra katika nyuga mbali mbali.

Bendera za Iran na Ghana

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii wa Ghana sanjari na kuwasilisha salamu za pongezi kwa Sayyid Raeisi kutoka kwa Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo amebainisha kuwa, anatumai kwamba, kwa kuondolewa vizuizi, uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu utaboreka kwa njia ya kipekee kuliko wakati wowote ule, hususan katika uga wa uchumi.

Amesema Ghana ni nchi ya kistratajia huko magharibi mwa Afrika, na kwamba nafasi yake hiyo ya kijiografia inaweza kutumiwa kama lango la kuingia katika nchi nyingine za Afrika na kuimarisha uhusiano wa kibiashara.