Spika Qalibaf: Japan ichukue hatua za maana za kuachiliwa fedha za Iran
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Japan ichukue hatua za maana kuhakikisha kwamba, fedha za Iran zilizozuiwa katika benki za nchi hiyo zinaachiliwa.
Dkt. Muhammad Baqir Qalibaf amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Toshimitsu Motegi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan na kueleza kwamba, Tehran inataraji kuiona serikali ya Tokyo ikichukua hatua za maana na kurahisisha njia ya kuachiliwa fedha za taifa hili hususan kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Japan inapaswa kuonyesha radiamali ya kimsingi kuhusiana na vikwazo vya dawa dhidi ya taifa hili.

Kadhalika amesema, masuala ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo mataifa haya mawili yanapaswa kuyazingatia.
Kwa upande wake, Toshimitsu Motegi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan ameashiria ulazima wa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na Japan na kubainisha kwamba, Tokyo ina hamu na shauku ya kuweko mazungumzo baina ya pande mbili katika uga wa masuala ya kiuchumi.
Aidha katika mazungumzo yake na Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan alisema ili kuyahuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani inapaswa kuachana na tabia yake ya uroho, uchu na hamu kubwa ya kukusanya na kurundika mali.