Iran yatuma ndege nyingine ya misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma ndege nyingine ya misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan kwa ajili ya kusaidiwa majeruhi na familia za Waislamu waliouliwa shahidi na kikatili wakiwa kwenye Sala ya Ijumaa huko Kunduz, kaskazini mwa Afghanistan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, ubalozi wa Iran nchini Afghanistan jana Jumatatu ulitangaza kuwa, ikiwa ni muendelezo wa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Afghanistan, Tehran imetuma ndege nyingine ya misaada ya kibinadamu kama vile madawa na vifaa vya matibabu kwa ajili ya kusaidiwa majeruhi na familia za Waislamu waliouliwa shahidi na kigaidi walipokuwa wanasali Sala ya Ijumaa Msikitini, huko kaskazini mwa Afghanistan.
Msikiti Mkuu wa wilaya ya Seyyedābad katika mkoa wa Kunduz wa Afghanistan ulishambuliwa na gaidi mkufurishaji aliyejiripua kwa mabomu siku ya Ijumaa na kupelekea zaidi ya Waislamu 100 kuuawa shahidi na wasiopungua 200 wengine kujeruhiwa.
Genge la kigaidi la Daesh au ISIS ndilo lililotangaza kuhusika na ukatili huo dhidi ya Waislamu waliokuwa kwenye Sala ya Ijumaa ndani ya Msikiti huo.
Shambulizi hilo linatajwa kuwa baya zaidi nchini Afghanistan tangu kundi la Taliban liliposhika tena madaraka ya nchi hiyo mwezi Agosti mwaka huu.
Wiki iliyopita pia, shehena ya tano ya misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasili mjini Kabul, Afghanistan ikiwa na tani 50 za chakula, madawa, mablanketi na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya wananchi wa Afghanistan.