Wanafunzi, wanavyuoni wa kidini Iran walaani mauaji ya Waislamu Afghanistan
Wahadhiri na wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran wamefanya maandamano makubwa ya kulaani ongezeko la mashambulio ya kigaidi yanayolenga misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan.
Mkusanyiko, vikao na maandamano ya kulaani hujuma hizo za umwagaji damu zilizowalenga waumini wasio na hatia tena wakiwa katika nyumba za ibada yalifanyika jana Jumapili katika Chuo cha Faizaya mjini Qum, ulioko umbali wa karibu kilomika 160 kusini Tehran, mji mkuu wa Iran.
Wanavyuoni na wanafunzi hao wa kidini wametoa mwito wa kulindwa roho na matukufu ya Kiislamu nchini Afghanistan, wakisisitiza kuwa hujuma hizo zinalenga kuibua mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Waislamu, katika misingi ya madhehebu.
Makumi ya watu wameuawa shahidi na mamia ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio kadhaa ya kigaidi dhidi ya misikiti ya Mashia nchini Afghanistan katika siku za hivi karibuni. Kundi la kigaidi la Daesh )ISIS) limetangaza kuhusika na mauaji na jinai hizo dhidi ya Waislamu wa Kishia.
Makumi ya watu waliokuwa katika Swala ya Ijumaa waliuawa shahidi na wengine karibu mia moja walijeruhiwa katika milipuko miwili iliyotokea Ijumaa iliyopita katika Msikiti wa Bibi Fatima katika mji wa Qandahar Afghanistan.
Aidha Ijumaa ya wiki iliyopita, Waislamu wasiopungua mia moja waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan na wengine karibu mia mbili walijeruhiwa.