Akiba ya urani iliyorutubishwa kwa 60% ya Iran yafikia kilo 25
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76580-akiba_ya_urani_iliyorutubishwa_kwa_60_ya_iran_yafikia_kilo_25
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema akiba ya madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini imefikia kilo 25.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2021 23:55 UTC
  • Akiba ya urani iliyorutubishwa kwa 60% ya Iran yafikia kilo 25

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema akiba ya madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 hapa nchini imefikia kilo 25.

Behrouz Kamalvandi alisema hayo jana Ijumaa hapa mjini Tehran katika maonyesho ya mafanikio ya Iran katika uga wa nyuklia na kuongeza kuwa, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu imefanikiwa kuzalisha kilo 210 ya urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20.

Amebainisha kuwa, hatua ya kuimarisha shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani imefanyika kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Bunge la Iran Disemba mwaka jana.

Wabunge wa Iran walipasisha kwa kishindo sheria inayofahamika kama "Mpango wa Kistratajia wa Kukabiliana na Vikwazo", na kuziagiza mamlaka husika za serikali kuchukua hatua zaidi za kupunguza uwajibikaji wa Iran katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa AEOI

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye uwezo wa kurutubisha urani kwa kiwango hicho cha asilimia 60.

Kamalvandi amesisitiza kuwa, "sekta ya nyuklia ni uga wenye nguvu, na ni chimbuko la mamlaka na fahari kwa taifa lolote lile. Madola ya kiistikbari hivi sasa yamefahamu kuwa hayawezi tena kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kustafidi na sekta hii."

Aprili mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu iliutumia barua Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ikiujulisha kuwa imeanza shughuli ya kuzalisha madini ya urani yaliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60.