Balozi wa Afrika Kusini Tehran ataka Iran iondolewe vikwazo
Balozi wa Afrika Kusini katika mji wa Tehran amesema kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran ni kwa maslahi ya jamii ya kimataifa. Ameongeza kuwa kuondolewa vikwazo hivyo kutakuwa na manufaa kwa nchi nyingi duniani.
Balozi Vika Mazwi Khumalo ameyasema hayo Ijumaaa katika mahojiano na Shirika la Habari la Iran, IRNA, kuhusu mabadilishano ya kibiashara na kisiasa baina ya Iran na Afrika Kusini. Ameendelea kusema kuwa: "Vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran vimepelekea kiwango cha kibiashara baina ya Afrika Kusini na Iran kushuka." Aidha amesema vikwazo hivyo vimesababisha mashirika makubwa ya Iran na Afrika Kusini kukumbwa na matatizo makubwa katika uga wa kibiashara.
Balozi Khumalo amebaini kuwa suala muhimu ni kuwa, Afrika Kusini haitambui rasmi vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran lakini pamoja na hayo mashirika makubwa ya kibinafsi yanajizuia kufanya biashara na Iran kwa kuhofia kuadhibiwa na Marekani.
Hali kadhalika amesema Iran na Afrika Kusini zina uhusiano mzuri sana wa kidiplomasia na maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili wamefanya vikao na kubadilishana mawazo katika kamisheni za pamoja za ushirikiano.
Balozi wa Afrika Kusini nchini Iran amesema kuna mustakabali mwema katika uhusiano wa kiuchumi baina ya Tehran na Pretoria na kueleza matumaini kuwa kutajiri matukio chanya katika mazungumzo ya nyuklia na hivyo kupelekea kufunguliwa milango ya uhusiano wa kibiashara baina ya nchi mbili.