Iran: IAEA iache pupa inapozungumzia masuala ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77028-iran_iaea_iache_pupa_inapozungumzia_masuala_ya_nyuklia
Kaimu Mwakilishi wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao huko Vienna, Austria ameziasa nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zijiepushe kutoa taarifa kwa haraka bila mazingatio juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 17, 2021 23:27 UTC
  • Iran: IAEA iache pupa inapozungumzia masuala ya nyuklia

Kaimu Mwakilishi wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao yao huko Vienna, Austria ameziasa nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zijiepushe kutoa taarifa kwa haraka bila mazingatio juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mohammadreza Ghayebi alitoa mwito huo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari mjini Vienna na kuongeza kuwa, nchi wanachama wa IAEA zinapaswa kujizuia kutoa taarifa za pupa na zilizochochewa na mielekeo ya kisiasa.

Amesema wakala huo wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yake ya hivi karibuni ulithibitisha kuwa unaendelea kufanya ukaguzi wake bila tashwishi katika vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amebainisha kuwa, ripoti hiyo ya IAEA ilieleza bayana kuwa, Iran imeendelea kufungamana na majukumu yake katika kutekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Grossi kuja Iran wiki ijayo

Kadhalika Ghayebi amebainisha kuwa, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi anatazamiwa kuitembelea Iran Jumatatu ijayo ya Novemba 22 kwa ziara rasmi ya kikazi.

Grossi anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI), Mohammad Eslami, miongoni mwa maafsa wengine.

Grossi anatazamiwa kuja nchini Iran siku chache kabla ya kuanza mazungumzo ya Vienna yenye lengo la kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.