Iran yasikitishwa na hali mbaya ya wakimbizi wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i77192-iran_yasikitishwa_na_hali_mbaya_ya_wakimbizi_wa_afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza wasi wasi wake kuhusu hali mbaya inayowakabili wakimbizi wa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 22, 2021 11:59 UTC
  • Iran yasikitishwa na hali mbaya ya wakimbizi wa Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza wasi wasi wake kuhusu hali mbaya inayowakabili wakimbizi wa Afghanistan.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo leo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran na kuongeza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na taasisi zote husika zimesimama na Waafghani katika kipindi chote, hususan nyakati za matatizo na changamoto.

Ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma misaada mbalimbali ya kibinadamu katika miji tofauti ya Afghanistan hususa katika kipindi hiki cha kukaribia msimu wa baridi kali.

Khatibzadeh amebainisha kuwa, katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya milioni nne wa Kiafghani, lakini mashirika ya kimataifa yamekataa kabisa kulisaidia taifa hili kuubebea mzigo wa kushughulikia maslahi ya wakimbizi hao.

Wakimbizi wa Kiafghani

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameashiria kuhusu safari ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambaye anatazamiwa kuwasili Tehran leo usiku na kubainisha kuwa, Tehran daima imekuwa ikiiasa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kusalia katika ushirikiano wa kiufundi na Iran.

Huku akieleza kuwa anatumai safari ya Grossi itakuwa chanya na yenye manufaa, Khatibzadeh amesema iwapo IAEA itajikita katika fremu ya utendajikazi wake, hakuna shaka hilo litazuia baadhi ya madola kufanikisha ajenda zao za kisiasa zinazoogemea upande mmoja. Mkurugenzi Mkuu wa IAEA anatembelea Iran siku chache kabla ya kuanza mazungumzo ya Vienna, yenye lengo la kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.