Dec 01, 2021 11:43 UTC
  • Taasisi ya Jiolojia ya Iran kuanza kazi magharibi mwa Afrika

Kufuatia kutiwa saini mapatano ya ushirikiano baina ya Taasisi ya Jiolojia na Uchimbaji Madini ya Iran na Taasisi ya Madini ya Mali, Iran sasa inatarajiwa kuimarisha shuhuli zake za jiolojia na uchimbaji madini magharibi mwa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa, mapatano hayo yametiwa saini hapa mjini Tehran na Abdoulaye Pona Mkurugenzi wa Taasisi ya Madini ya Mali alipotembelea kitengo cha utafiti cha  Taasisi ya Jiolojia na Uchimbaji Madini ya Iran.

Kwa mujibu wa mapatano hayo ambayo yalitiwa saini kwa upande wa Iran na Alireza Shahidi, ambaye ni mkurugenzi wa Taasisi ya Jiolojia na Uchimbaji Madini ya Iran, kutakuwa na mabadilishano ya uzoefu, utaalamu wa kisayasni, utafiti na ufundi.

Hali kadhalika pande mbili zitashirikiana katika kutayarisha ramani za kijiolojia na uchimbaji madini kwa kutumia teknolojia za kisasa na za kimataifa.

Utiaji saini mapatano ya madini baina ya Iran na Mali

Hussein Talashia Salehani, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Mali ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa pande mbili walioshiriki katika utiaji saini huo.

Hivi karibuni pia Shirika la Uhandisi wa Madini la Iran na Idara ya Uchimbaji Madini la Mali zilitiliana saini mapatano ya ushirikiano.

Mali ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini ambao umekuwa ukiporwa kwa muda mrefu na madola ya kikoloni hasa Ufaransa ambayo iliikoloni nchi hiyo. 

Tags