Jahromi: Uingereza imesalimu amri mbele ya nguvu za taifa la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81488-jahromi_uingereza_imesalimu_amri_mbele_ya_nguvu_za_taifa_la_iran
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya kupita miaka 40 ya kutotekeleza ahadi zake, hatimaye Uingereza imesalimu amri mbele ya nguvu za mazungumzo za taifa la Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2022 07:25 UTC
  • Jahromi: Uingereza imesalimu amri mbele ya nguvu za taifa la Iran

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baada ya kupita miaka 40 ya kutotekeleza ahadi zake, hatimaye Uingereza imesalimu amri mbele ya nguvu za mazungumzo za taifa la Iran.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ali Bahadori Jahromi akisema hayo leo Alkhamisi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuandika: Kwa mara nyingine tena taifa la Iran limepata ushindi katika vita vya msimamo usiotetereka. Baada ya miaka 40 ya ahadi chapwa isizotekeleza, hatimaye Uingereza imeilipa Iran deni lake la dola milioni 530 ilizokuwa imekataa muda wote huu kuzilipa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian amesema, deni ambalo taifa la Iran lilikuwa linaidai Uingereza limelipwa, lakini malipo hayo hayana mfungamano wowote na kuachiwa huru na Iran watu waliokuwa wametiwa mbaroni humu nchini kwa masuala ya usalama.

Kifaru cha Chieftain

 

Nazanin Zargari na Anoosheh Ashoori, raia wawili wa Iran ambao pia wameomba uraia wa Uingereza, walikamatwa nchini Iran kwa kufanya vitendo vya ujasusi. Jana Jumatano majasusi hao walikabidhiwa kwa Uingereza baada ya kutumikia adhabu zao za kifungo hapa Iran.

Mwaka 1976 kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, utawala kibaraka wa Shah wa Iran uliilipa Uingereza karibu dola bilioni moja kwa ajili ya kununuliwa vifaru ya Uingereza aina ya Chieftain. Mkataba huo wa karibu miaka 50 iliyopita, ulitiwa saini mwaka 1971 na ulikuwa ni wa kuuziwa Iran vifaru hivyo 1500 vya Uingereza.

Uingereza iliipa Iran vifaru 150 tu na baada ya kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 humu nchini, Uingereza haikuipa tena Iran vifaru vyake.