Mar 23, 2022 06:36 UTC
  • Takht Ravanchi: Tupateni ilhamu katika ujumbe wa amani, urafiki, mshikamano na upendo wa Nouruzi

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, "tupateni ilhamu katika ujumbe wa amani, urafiki, mshikamano na upendo wa Nouruzi."

Majid Takht Ravanchi ametoa mwito huo katika sherehe ya Nouruzi iliyofanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa, jijini New York.

Kwa ubunifu na uongozi wa ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa na kwa ushiriki wa nchi zingine 11 za eneo la Nouruzi, kikao cha kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nouruzi kimefanyika kwa njia ya intaneti katika makao makuu ya umoja huo.

Kikao hicho kilichofanyika kwa uwenyekiti wa balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran Umoja wa Mataifa, kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Rais wa Baraza Kuu na Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la umoja huo.

Kitanga cha vitu Saba vyenye majina yaanzayo na "Sin" cha Nouruzi na bendera za nchi za eneo la Nouruzi

Katika hotuba aliyotoa kwenye kikao hicho, Takht Ravanchi amesema, "katika dunia ambayo mwanadamu anakabiliana na changamoto zisizohesabika na nadra kuwahi kushuhudiwa, kama janga la dunia nzima la corona, uchukuaji misimamo ya upande mmoja, misimamo ya kufurutu mpaka, ukatili, uadui na mizozo, njooni tuchukue ilhamu kwenye Nouruzi na jumbe zilizomo ndani yake kama amani, urafiki, mshikamano na upendo."

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran UN ameongeza kuwa, Nouruzi si tu ni daraja madhubuti la kuunganisha zama zilizopita, za sasa na zijazo, lakini pia ni nembo ya kulinda thamani, tunu na malengo matukufu ya pamoja, sambamba na kuheshimu mchanganyiko wa tamaduni ambazo huhamishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika zama zote za historia.../

Tags