Ershadi: Vikwazo vinatishia haki ya tiba ya wananchi wa Iran
Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni tishio kubwa kwa haki ya kupata huduma za afya, matibabu na dawa wananchi wa Iran.
Zahra Ershadi alisema hayo jana Jumanne katika mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa ukijadili mfumo wa afya wa dunia na sera za kigeni.
Amesema huduma za afya za bei nafuu pamoja na madawa ya kuokoa maisha na teknolojia za matibabu zinapaswa kupatikana kiwepesi katika nchi zote duniani pasi na ubaguzi wala kuzingatia misimamo ya kisiasa.
Amesisitiza kuwa, kuwekewa vikwazo vya upande mmoja wananchi wa Iran hususan vikwazo vya dawa na bidhaa nyinginezo ni jinai na uhalifu sawa na jinai dhidi ya binadamu.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, vikwazo hivyo vinavyokiuka sheria vina taathira hasi na ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi walio hatarini zaidi wa Iran wakiwemo wanawake, watoto na wagonjwa.
Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, masuala ya afya hayapaswi kufanyiwa siasa hata kidogo, na kufanya hivyo ni kuyaweka hatarini maisha ya raia wasio na hatia.