Iran: Utawala wa Kizayuni ndio tatizo kuu la Ulimwengu wa Kiislamu
-
Hossein Amir-Abdollahian
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio tatizo kuu la Ulimwengu wa Kiislamu.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Qatar, Muhammad bin Abdurahman al-Thani pembeni ya mkutano wa majirani wa Afghanistan unaofanyika katika mji wa Tunxi China.
Ameeleza kuwa, kufanyika Kikao cha Uovu Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Naqb) ni usaliti mkubwa kwa malengo matukufu ya Palestina na akaongezea kwa kusema: "kwa masikitiko, baadhi ya nchi za eneo zinaendelea kuchukua hatua ya kihaini ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huu wa Israel, licha ya hatua hiyo kukinzana na malengo aali na matukufu ya Waislamu duniani kuhusiana na Quds tukufu na Palestina.
Siku ya Jumapili iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne za Kiarabu za Misri, Imarati, Bahrain na Morocco walishiriki katika mkutano maalumu uliohudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu la Naqab.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia kuhusu uwezo na fursa zilizopo katika uga wa mashirikiano ya pande mbili za Iran na Qatar katika sekta ya uchumi; na akatilia mkazo kufuatiliwa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi mbili.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdurahman al Thani, naye pia ametilia mkazo kustawishwa uhusiano wa pande mbili sambamba na umuhimu wa kusimamiwa amani ya eneo kwa ushiriki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema, ana matumaini kuwa nchi zote za eneo zitafanya jitihada kwa ajili ya kuleta uthabiti na kusimamia amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi.../