Iran iko tayari kwa vita vya muda mrefu na Marekani
Kamanda mwandamizi wa kijeshi Iran amesema, Tehran iko tayari kwa vita vigumu na Marekani.
Brigedia Jenerali Massoud Jazayeri, Naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran ametoa kauli hiyo baada ya mgombea uteuzi wa kiti cha urais kwa tiketi ya Wademocrat Marekani Hillary Clinton kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran endapo atachaguliwa. Katika hotuba yake yenye misimamo mikali kuhusu sera za kigeni aliyoitoa siku ya Alkhamisi, Clinton alisema eti Marekani inaweza kuipokonya Iran silaha zake kupitia vta.
Akijibu kauli hiyo iliyojaa kiburi, Brigedia Jenerali Jazayeri alisema, "Ingawa kauli za machaguo yote yako mezani" dhidi ya Iran ni propaganda za kimaonyesho za Marekani, lakini pamoja na hayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kwa vita vigumu na vya "kuainisha hatima" baina yake na Marekani."
Amesema Iran kamwe haijawahi kuanzisha vita na nchi yoyote ile lakini wakati huo huo haijawahi kupuuza uwezo wajibu wake wa kujiimarisha kijeshi.
"Iwapo Marekani itatekeleza vitisho vyake, Wairani wako tayari kuwaondolea wanadamu shari ya kupenda vita ya Marekani na sera zake za kibeberu katika vita vya ana kwa ana," ameongeza.
Jazayeri pia amekosoa matamshi ya rais Barack Obama wa Marekani ambaye amedai eti anasikitika kuona namna Wasyria walivyopoteza maisha na nchi yao kuharibiwa vitani.
Kamanda huyo wa kijeshi Iran amesema, Marekani inahusika katika kuwapa silaha magaidi wakufurishaji wakiwemo wa ISIS yaani Daesh nchini Syria ambao wamekuwa wakifanya mauaji ya kidhalimu dhidi ya Wasyria kwa miaka sita sasa. Amesema muungano unaongozwa na Marekani wa eti kupambana na Daesh (ISIS) haujawa na chochote isipokuwa kuwa kuendelea kuwapa magaidi misaada ya silaha ili waendeleze vita dhidi ya serikali na watu wa Syria.