Rais Ebrahim Raisi: Nchi huru zishirikiane ili kusambaratisha vikwazo vya mabeberu
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ushirikiano baina ya nchi huru katika kudhamini mahitaji yao ya pamoja kieneo na kimataifa ni jambo muhimu sana na ndiyo njia ya kusambaratisha mashinikizo ya madola yanayopenda kuziwekea vikwazo nchi nyingine.
Rais Raisi alisema hayo jana katika mazungumzo ya simu na Rais Vladimir Purin wa Russia na kuelezea matumaini yake ya kumalizika haraka mgogoro wa Ukraine akisisitiza kuwa, njia ya kutatua mgogoro huo ni mazungumzo ya kidiplomasia.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutumia ushawishi na uwezo wake wote kusaidia utatuzi wa kidiplomasia wa vita vya Ukraine.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia njama za baadhi ya nchi za Magharibi za kupasisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kuongeza kuwa, pamoja na matukio ya kimataifa, Tehran inafanya juhudi za kuimarisha uhusiano wake wa pande zote na nchi huru duniani.

Pia amesema kwa mara chungu nzima wakala wa IAEA umesisitiza kuwa Iran haijakengeuka kivyovyote vile mradi wake wa amani wa nyuklia na kwamba sasa hivi ni Marekani ndiyo inayopaswa kuchukua uamuzi wa kufufua mapatano ya nyuklia kwani msimamo wa Iran uko wazi katika jambo hilo na sio kupasisha azimio dhidi ya Iran.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia ameelezea kuhuzinishwa na ajali ya treni iliyoua na kujeruhi raia kadhaa wa Iran na ametilia mkazo wajibu wa kushirikiana zaidi kiuchumi na kibiashara nchi mbili jirani za Iran na Russia.
Pia amesema, kuna udharura wa nchi hizi mbili kushirikiana zaidi katika mabadilishano ya kibenki, usafirishaji bidhaa, nishati na masuala ya kilimo.