Iran kati ya nchi 15 zinazovutia idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni
Iran imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 15 duniani, zenye kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni.
Hayo yamesemwa leo na Mohammad-Javad Salmanpur, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayehusika na Masuala ya Sayansi na kuongeza kuwa, katika mwaka uliopita wa Kiirani (Baina ya Machi 2021 na Machi 2022), idadi ya wanafunzi waliokubaliwa kujiunga na Vyuo Vikuu vya Iran iliongezeka maradufu.
Amesema Vyuo Vikuu vya Iran vinapokea idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani, ikilinganishwa na vyuo vingine hasimu katika eneo na hata barani Ulaya.
Salmanpour ameeleza kuwa, kuna ushindani mkubwa wa Vyuo Vikuu katika eneo kuwavutia wanachuo wa nchi za kigeni, na hilo limetokana na ujio wa vyuo vipya katika nchi kama Uturuki, Imarati, Russia, Saudia, Jordan na Misri.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayehusika na Masuala ya Sayansi amebainisha kuwa, kuna wanafunzi zaidi ya laki moja (100,000) wa kigeni katika Vyuo Vikuu vya Iran. Ameongeza kuwa, asilimia 90 ya wanachuo hao wa kigeni walioko Iran ni kutoka Afghanistan na Iraq.
Amesema kuna wanafunzi 95,000 wa Kiirani wanaosoma katika Vyuo Vikuu vya nchi mbalimbali duniani, wakiwemo 12,000 wanaosomea nchini Uturuki.